Matthew 17

Isa Abadilika Sura Mlimani

(Marko 9:2-13; Luka 9:28-36)

1 aSiku sita baada ya jambo hili, Isa akawachukua Petro, Yakobo na Yohana ndugu yake Yakobo, akawapeleka juu ya mlima mrefu peke yao. 2 bWakiwa huko, Isa alibadilika sura mbele yao. Uso wake ukang’aa kama jua na nguo zake zikawa na weupe wa kuumiza macho. 3Ghafula wakawatokea mbele yao Musa na Ilya, wakizungumza na Isa.

4Ndipo Petro akamwambia Isa, “Bwana, ni vyema sisi tukae hapa. Ukitaka, nitafanya vibanda vitatu: kimoja chako, kingine cha Musa na kingine cha Ilya.”

5 cPetro alipokuwa angali ananena, ghafula wingu lililong’aa likawafunika, na sauti ikatoka kwenye hilo wingu ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa. Ninapendezwa naye sana. Msikieni yeye.”

6 dWanafunzi waliposikia haya, wakaanguka chini kifudifudi, wakajawa na hofu. 7 eLakini Isa akaja na kuwagusa, akawaambia, “Inukeni na wala msiogope.” 8Walipoinua macho yao, hawakumwona mtu mwingine yeyote isipokuwa Isa.

9 fWalipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Isa akawaagiza, “Msimwambie mtu yeyote mambo mliyoyaona hapa, mpaka Mwana wa Adamu atakapofufuliwa kutoka kwa wafu.”

10 gWale wanafunzi wakamuuliza, “Kwa nini basi walimu wa sheria husema kwamba ni lazima Ilya aje kwanza?”

11 hIsa akawajibu, “Ni kweli, Ilya lazima aje kwanza, naye atatengeneza mambo yote. 12 iLakini nawaambia, Ilya amekwisha kuja, nao hawakumtambua, bali walimtendea kila kitu walichotaka. Vivyo hivyo Mwana wa Adamu pia atateswa mikononi mwao.” 13 jNdipo wale wanafunzi wakaelewa kuwa alikuwa anazungumza nao habari za Yahya Mbatizaji.

Isa Amponya Kijana Mwenye Pepo

(Marko 9:14-29; Luka 9:37-43)

14 kWalipofika penye umati wa watu, mtu mmoja akamjia Isa na kupiga magoti mbele yake, akasema, 15 l“Bwana, mhurumie mwanangu. Yeye ana kifafa na anateseka sana. Mara kwa mara huanguka kwenye moto au kwenye maji. 16Nilimleta kwa wanafunzi wako, lakini hawakuweza kumponya.”

17 mIsa akajibu, “Enyi kizazi kisichoamini na kilichopotoka! Nitakaa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni mvulana hapa kwangu.” 18Isa akamkemea yule pepo mchafu, akamtoka yule kijana, naye akapona saa ile ile.

19 nKisha wanafunzi wakamwendea Isa wakiwa peke yao, wakamuuliza, “Kwa nini sisi hatukuweza kumtoa?”

20 oAkawajibu, “Kwa sababu ya imani yenu ndogo. Ninawaambia kweli, mkiwa na imani ndogo kama punje ya haradali, mtauambia mlima huu, ‘Ondoka hapa uende pale,’ nao utaondoka. Wala hakutakuwa na jambo lisilowezekana kwenu. [ 21Lakini hali kama hii haitoki ila kwa kuomba na kufunga.]”

22 pSiku moja walipokuwa pamoja huko Galilaya, Isa akawaambia, “Mwana wa Adamu atasalitiwa na kutiwa mikononi mwa watu. 23 qNao watamuua, lakini siku ya tatu atafufuliwa.” Wanafunzi wakahuzunika sana.

Isa Na Petro Watoa Kodi Ya Hekalu

24 rBaada ya Isa na wanafunzi wake kufika Kapernaumu, wakusanya kodi ya Hekalu
Kodi ya Hekalu ilikuwa didrachmas, yaani drakma mbili, ambazo ni sawa na nusu shekeli.
wakamjia Petro na kumuuliza, “Je, Mwalimu wenu halipi kodi ya Hekalu?”

25 tPetro akajibu, “Ndiyo, yeye hulipa.” Petro aliporudi nyumbani, Isa akawa wa kwanza kulizungumzia, akamuuliza, “Unaonaje Simoni? Wafalme wa dunia hupokea ushuru na kodi kutoka kwa nani? Je, ni kutoka kwa watoto wao au kutoka kwa watu wengine?”

26Petro akamjibu, “Kutoka kwa watu wengine.” Isa akamwambia, “Kwa hiyo watoto wao wamesamehewa. 27 uLakini ili tusije tukawaudhi, nenda baharini ukatupe ndoana. Mchukue samaki wa kwanza utakayemvua. Fungua kinywa chake nawe utakuta humo fedha, ichukue ukalipe kodi yako na yangu.”
Copyright information for SwhKC